Dar
es Salaam. Tanzania na Sri Lanka zimetiliana saini mikataba ya
ushirikiano kwenye maeneo ya uchumi na utalii,huku Rais Jakaya Kikwete
akiliombea amani taifa hilo ambalo linakabiliwa na hali mbaya ya
kisiasa.
Makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ikulu mbele ya
marais wote wawili Rais Kikwete na mgeni wake Mahinda Rajapaska yanahusu
ushirikiano kwenye eneo la biashara kwa kuanzisha vitega uchumi
vitavyowajumuisha wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Pia makubaliano hayo yamelenga kuimarisha sekta ya
utaliii,ambapo imekubaliwa kuwa kila upande utatumia rasilimali zake
kuwavutia watalii na kwamba kwa kuanzia ujumbe wa Tanzania unatazamia
kutembelea Sri Lanka baadaye mwaka huu kwa ajili ya kufanya tathimini.
Akizungumzia hatua ya kutiwa saini makubaliano
hayo ambayo pia yanahusu eneo la utamaduni, Waziri wa Mambo ya Nchi za
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema nchi zote mbili
zinategemea kunufaika hasa kwa kuzingatia kuwa makubaliano hayo
yamefanyika kwa kuzingatia historia ya nchi zote.
“ Sasa tumefungua ukurasa mpya.. tunategemea kuona
watanzania wakimiminika kwa wingi nchini Sri Lanka kwa ajili ya
kutafuta fursa za kibiashara” alisema Membe.
Akizungumza kwenye hafla maalumu ya chakula cha
jioni aliyomwandalia mgeni wake, Rais Jakaya Kikwete alipongeza hatua
zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya Sri Lanka kwa ajili ya
kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo pia kukabiliana na mawimbi
mabaya ya kisiasa.
“ Ni matumaini yangu hali ngumu ya kisiasa
inayojitokeza sasa itapatiwa ufumbuzi na hatimaye taifa hili litaendelea
kuangaza. Naamini mtaendelea kupiga hatua kwenye maeneo ya uchumi na
maendeleo kwa ujumla” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Rais wa Sri Lanka Mahinda
Rajapaska pamoja na kupongeza ushirikiano wa pande zote mbili lakini pia
alielezea matumaini yake kuhusiana na hatua ya ukuzaji uchumi.
Alisema serikali zote zitaendelea kushirikiana
kukabiliana na matukio yanayoendelea kutokea duniani ikiwemo pia
kukabiliana na vitendo vya ugaidi


No comments:
Post a Comment