Dar es Salaaam. Chama cha Wananchi (CUF)
kimeahirisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu kwa
sababu Rais Jakaya Kikwete, atakuwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Smart
Partnership na kushughulikia ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani.
Maandamano hayo yalikuwa na lengo la kumfikishia
Rais Kikwete ujumbe kuhusu vitendo vya ukatili, wizi, ubakaji na mauaji
vinavyofanywa na polisi mkoani Mtwara na kutaka uchunguzi kuhusu matukio
ya Arusha.
Hata hivyo kuahirishwa kwa maandamano hayo
kunakuja baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova kupiga
marufuku maandamano ya aina yoyote na kwamba polisi watapambana na
yeyote atakayakaidi amri hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema: “Tumepokea barua kutoka
Ikulu, kutuomba tusitishe maandamano hayo kwa sababu Rais ambaye ndiye
mpokeaji wa maandamano hayo atapokea wageni mbalimbali watakaoingia
nchini,” alidai.
Mtatiro alisema barua hiyo ilieleza kuwa
haitawezekana Rais kupokea maandamano ya CUF kwa kuwa atakuwa akipokea
wageni mbalimbali.
“Sisi tulimwandikia Rais barua kuwa Juni 29 mwaka
huu tutakuwa na maandamano ya kuelekea Ikulu,hatukujua kama kutakuwa na
ugeni wa marais siku hiyo...tumeahirisha,”alisema

No comments:
Post a Comment