Powered By Blogger

Translate

Monday, July 15, 2013

JESHI LA KENYA LA KANUSHA UPORAJI MAKAA YA MAWE SOMALIA

Jeshi la Kenya limekanusha madai kuwa limekuwa likipora raslimali ya Somalia kwa kuhusika na uuzaji wa makaa katika mji wa bandari wa Kismayo.
Ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa inaishtumu jeshi la Kenya kwa kuuza makaa nje ya Somalia kinyume na sheria katika Bandari hiyo ya Kisimayo.
Kamati kuu ya usalama ya Umoja wa Mataifa ilikuwa imepiga marufuku uuzaji wa bidhaa zote zinazoshukiwa kuwa vitega uchumi wa kundi la wapiganaji wa kiislamu la al Shabab kuanzia mwezi februari mwaka uliopita, ili kuzuia wapiganaji hao wa waasi kupata fedha za kufadhili shuguhuli zao ikiwa ni pamoja na ununuzi wa silaha na kuwalipa mishahara wapiganaji wake.
Bandari hiyo ya Kismayo iko chini ya jeshi la umoja wa Afrika kwa pamoja na serikali ya Somalia tangu ilipokombolewa kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu wa Al Shabaab.
Jeshi la Kenya kwa sasa ndilo linalohudumu mjini Kismayo na katika maeneo kadhaa ya Kati na Kusini mwa Somalia.

UCHUNGUZI MAUAJI YA WANAJESHI



Msemaji Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu askari wa kulinda amani wa Tanzania waliouawa Dafur, Sudan.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kulinda Amani, Meja Sadala Kapungu. 
0
Share
Dar es Salaam. Wakati Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban K-Moon, wamelaani mauaji ya wanajeshi wa Tanzania Jimbo la Darfur, Sudan,  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeunda timu ya kuchunguza tukio hilo.
Wapiganaji saba kati ya 36 wa Tanzania waliokuwa kwenye Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa, (Unamid), waliuawa  Jumamosi na wengine 19 kujeruhiwa.
Mashambulizi hayo yalitekelezwa karibu na kambi ya Manawashi eneo la Khor Abeche, mji wa Darfur Jimbo la Nyala.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema Dar es Salaam jana kuwa timu ya wataalamu itakwenda Darfur kuchunguza tukio hilo.
Tukio hilo limekuwa la kushtua, kwani miaka mitano ya majeshi ya kulinda amani kuwa huko haijawahi kutokea mauaji makubwa kiasi kile.
 Kanali Mgawe alisema wanawasiliana na UN kufanya taratibu za kurudisha nyumbani miili ya wapiganaji hao.
Taarifa ya Unamid
Taarifa ya iliyotolewa jana na Msemaji wa Unamid, Christopher Cycmanick,   ilisema wanajeshi hao waliuawa walipokuwa kwenye doria ya kawaida.
Cycmanick alisema walinzi hao wa amani walishambuliwa kwa bunduki na silaha nzito za kivita umbali wa kilomita 25 kutoka katika kambi yao.
JK atuma salamu za pole
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Rais Kikwete ameeleza kushtushwa na tukio la kushambuliwa na kuuawa wapiganaji wa JWTZ Mji wa Darfur, Sudan.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu, ilisema Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, familia na wapiganaji wote.

CHADEMA KIDEDEA



Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)wakiimarisha ulinzi kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kaloleni wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo uliofanyika jana.Picha na Filbert Rweyemamu. 

Posted  Jumatatu,Julai15  2013  
Kwa ufupi
  • Yaibuka na ushindi wa kishindo katika kata zote nne za Arusha Mjini, wapiga kura  wengi washindwa kujitokeza
Arusha. Chadema kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470 dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha 15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu kukitetea kiti hicho.