Powered By Blogger

Translate

Monday, July 8, 2013

MACHINGA MSIDANGANJIKE


Askari Polisi na Mgambo wa Jiji wakiimarisha ulinzi katika eneo lamanzese jijini Dar es salaam jana, baada ya kutokea vurugu kati ya mgambo na Wamachinga zilizosababisha barabara ya Morogoro kufungwa kwa muda kwa saa tatu. 

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana amewataka wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kutodanganywa  na wanasiasa kwa lolote kwani mpango wa kuwaondoa maeneo wasiyotakiwa ni wa lazima. “Leo tunaendelea mitaa ya Manzese, Ubungo na hata Mwenge kwani ni lazima waondoke ili kazi za umma zifanyike’’ alisema.
Kauli ya Rugimbana imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kutokea vurugu za wafanyabiashara na polisi wa kutuliza ghasia na mgambo wa jiji waliokuwa wakiwataka kuondoka katika eneo hilo ili kutoa nafasi ya mradi wa ujenzi wa barabara wa mabasi yaendayo kasi (BRT) eneo hilo.
Rugimbana alisema baadhi ya wanasiasa wanatumia majukwaa yao vibaya kwa kuwadanganya wafanyabiashara hao hilo zoezi la kuhamishwa eneo la Manzese ilikuwa ni la muda mfupi kwa ajili ya ujio wa Rais Barack Obama. Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Rugimbana alisema zoezi la kuwahamisha wamachinga hao ni la kisheria kwa sababu  lazima waondoke ili kumpisha mkandarasi aendelee na ujenzi wa barabara hiyo.
“Tuna mgongano na baadhi ya wanasiasa ndio wanaoturudisha nyuma wanawapotosha hawa wamachinga, sisi tunafuata sheria sio siasa lazima waondoke ili mkandarasi aendelee kufanya kazi eneo lile,” alisema Rugimbana.
Rugimbana  alisema  zoezi hilo ni endelevu hivyo yeyote atakayeenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria hivyo wametakiwa kuondoka eneo hilo.
Alisema wafanyabiashara hao kama wana matatizo wanatakiwa wamuone mkuu huyo, Meya wa manispaa hiyo ili waweze kukaa pamoja na kutatua matatizo yao.
“Hili zoezi ni endelevu na leo hii oparesheni itaendelea maeneo yote ambayo hayaruhusiwi kama Ubungo, Manzese na Mwenge, kama eneo la Mwenge tumewaondoa wafanyabiashara na vibanda vyao vimebomolewa  ili kupisha upanuzi wa barabara,”

HATIMA YA MAKAMANDA WA CHADEMA KUJULIKANA TABORA

Dar es Salaam. Hatima ya makada watano wa Chadema, wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, inatarajiwa kujulikana leo, wakati mahakama hiyo itakapotoa uamuzi kuhusiana na kesi hiyopamoja na mambo mengine, uhalali wa mashtaka yanayowakabili.
Makada hao wa Chadema, Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni,  Evodius Justinian, Oscar Kaijage,  Rajabu Daniel, Seif Magesa Kabuta, walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mawili, moja la ugaidi na lingine la jinai.
Katika shtaka la kwanza wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora,  na la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu wakidaiwa kumdhuru Tesha kwa kumwagia tindikali.
Walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mawakili wao, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari walipambana kuwanusuru na mashtaka hayo.
Mawakili hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo,wakidai kuwa hakuna vigezo vya kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji utaratibu wa kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule walikokamatiwa.
Hivyo waliiomba Mahakama hiyo ama iwafutie mashtaka hayo au iamuru kila mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika mahakama za mahali walikokamatiwa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Juma Masanja akisaidiana na Wakili wa Serikali, Idelfonce Mukandara, walidai mashtaka hayo ni halali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Joctan Rushwera aliahirisha kesi hiyo na kupanga kutoa uamuzi leo.
Hakimu Rushwera aliamuru washtakiwa wote wapelekwe mahabusu wakisubiri uamuzi wa kesi yao leo, kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.

WAFA KWA MAANDAMANO MISRI

Takriban watu 15 wameuawa mjini Cairo kufuatia ghasia nje ya kambi ya kijeshi ambapo wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi wanaamini kiongozi huyo anazuiliwa.
Haya yanajiri huku ghasia zikiendelea baada ya kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa rais Mohammed Morsi.
Waandamanaji hao wanasema vikosi maalum viliwafyatua risasi baada ya swala ya fajir huku wengine wakishambuliwa walipokusanyika nje ya makao ambako bwana Morsi anadhaniwa kuzuiliwa wakitaka watawala kumwachilia huru.
Msemaji wa chama cha Muslim brotherhood amesema kuwa idadi ya waliofariki katika ghasia hizo imefikia 30 huku zaidi ya watu 500 wakijeruhiwa.
Lakini katika taarifa yake, jeshi la nchi hiyo limesema kuwa kundi moja la kigaidi lilikuwa likijaribu kuingia katika kambi hiyo na kumuua mwanajeshi mmoja.
Limeongezea zaidi ya watu 200 walitiwa mbaroni wakimiliki silaha kama vile visu.
Duru kutoka wizara ya afya zilisema kuwa afisaa mmoja wa jeshi aliuawa.
Bwana Morsi, aliyekuwa rais wa kwanza wa kiisilamu kuchaguliwa kidemopkrasia Misri, aling'olewa mamlakani na jeshi, siku ya Jumatano baada ya kufanyika maandamano makubwa.
Mmoja wa waandamanaji Mahmud al-Shilli, aliambia shirika la habari la AFP kuwa wanajeshi waliwarushia gesi ya kutoa machozi lakini kikundi cha wanaume waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia ndio waliwafyatulia risasi.
Katika taarifa iliyosomwa kwenye vyombo vya habari vya serikali, jeshi lililaumu kikundi cha watu walaiokuwa wamejihami ambao limesma ni mgaidi waliokuwa na njama ya kuvamia kambi ya jeshi.