Powered By Blogger

Translate

Sunday, July 14, 2013

Mbowe adai polisi walivamia usiku makazi yake D’Salaam

Dar es Salaam. Polisi kadhaa wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa lengo la kumkamata.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mbowe mwenyewe zinaeleza kuwa askari hao waliokuwa na silaha walivamia nyumba hiyo iliyopo eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana wakiwa na silaha.
Mbowe alisema hata hivyo walikwama kumkamata, kwa sababu alikuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za chama.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikataa kuzungumzia zaidi suala hilo akieleza kuwa anayeweza kulizungumzia zaidi ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillius Wambura alipoulizwa alisema kuwa hana taarifa za polisi kumtafuta Mbowe.
“Sina taarifa polisi wangu kumtafuta Mbowe,” alisema Wambura.
Lakini Ofisa Habari wa Chadema Tumaini Makene aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa askari hao walifika nyumbani kwa Mbowe saa 7:16 usiku, wakidai kuwa na hati ya kumkamata Mbowe kutokana na makosa ambayo hata hivyo hawakuyabainisha.
“Ni kweli askari walifika nyumbani kwa Mwenyekiti wakidai walikuwa wakihitaji kumkamata. Kinachotushangaza ni kwamba mtu ambaye anafahamika na wanajua ni mbunge na kiongozi wa chama, lakini wanakwenda kumkamata kama jambazi, usiku wa manane,” alisema Makene.
Alisema kuwa polisi hao walifika nyumbani kwa Mbowe na kukutana na walinzi katika nyumba hiyo, waliowaeleza kuwa mwenyekiti huyo wa Chadema alikuwa safarini.
Makene hakuwataja majina walinzi waliokutwa , lakini nalisisitiza kwamba polisi hao waliacha namba za simu kwa walinzi hao, wakitoa maelezo kuwa pindi Mbowe atakaporejea wamwarifu na kuwapigia polisi kwa kuwa alikuwa akihitajika kituoni.
Ofisa huyo alieleza kuwa wakati wa tukio hilo Mbowe hakuwapo nyumbani na alikuwa safarini mkoani Kilimanjaro, kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Hai.
Makene alisema wanashangazwa na vitendo vya Polisi kusaka viongozi wao usiku wa manane kama majambazi sugu, wakati wakifahamika ni wabunge.

UCHAGUZI ARUSHA VURUGU ZATAWALA

Masanduku ya kuhesabia kura uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha 
Kwa ufupi
Mbali ya NEC kupiga marufuku viongozi hao wa kisiasa kukaribia vituo hivyo, uchaguzi huo umekumbwa na matukio kadhaa likiwamo la Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Taifa Chadema(Bavicha), John Heche, kunusurika kuswekwa rumande jana
0
Shar
Arusha. Uchaguzi mdogo katika kata nne za Jiji la Arusha unafanyika leo, huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikiwapiga marufuku Mkuu wa Mkoa, Magessa Mulongo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongella kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, wala kujihusisha kwa namna yoyote na zoezi la upigaji kura ikisema siyo jukumu lao kisheria.
Mbali ya NEC kupiga marufuku viongozi hao wa kisiasa kukaribia vituo hivyo, uchaguzi huo umekumbwa na matukio kadhaa likiwamo la Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Taifa Chadema(Bavicha), John Heche, kunusurika kuswekwa rumande jana.
“RC na DC hawana haki wala mamlaka ya kujihusisha kwenye zoezi na shughuli za upigaji kura. Mwenye dhamana, wajibu na haki ya shughuli zote za upigaji kura ni Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni mwakilishi wa NEC pamoja na maofisa wengine wanaotambuliwa kisheria,” alisema Mwenyekiti wa NEC Jaji Damian Lubuva jana.
Lema na Heche walinusurika kuswekwa rumande baada ya kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha, wakishinikiza jeshi hilo, kukamata magari matatu waliyodai kuwa ni ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kubadilishwa namba yakihofiwa kwamba huenda yakatumika kuvuruga uchaguzi wa leo.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea jana asubuhi baada ya viongozi hao, kufika polisi na kutoa taarifa hiyo, wakieleza kuwa lakini waliambiwa waondoke kwa kuwa gari kubadili namba siyo kosa ambapo pia walitakiwa kumtaja aliyewaeleza kama magari hayo yatatumika kufanya uhalifu.
Aidha, viongozi wa vyama vyote vya siasa ambao sio mawakala wala wagombea, wamepigwa marufuku kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, wala kujihusisha kwa namna yoyote na zoezi la upigaji kura badala yake wakiwa ni wakazi wa kata husika kupiga kura na kuondoka maeneo hayo.
Mwenyekiti wa NEC, alitoa tamko la kuzuia viongozi hao jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mipango na mikakati ya tume yake katika kufanikisha zoezi hilo linalofanyika baada ya kuahirishwa mara mbili.
Mbele ya makamu wake Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Jaji Hamid Mohamoud Hamid, Jaji Lubuva alitaja orodha ya watu 12 wenye haki kisheria kuingia kwenye vituo vya kupigia kura na kujihusisha na zoezi la upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura kuwa ni msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi wa kituo, mawakala wa vyama na wapiga kura.
Wengine ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, mgombea, mjumbe wa NEC, Ofisa wa NEC, Mratibu wa NEC mkoa, askari polisi au mtu yeyote anayehusika na usalama katika kituo cha kupiga kura, mtu anayemsaidia mpigakura asiyejiweza na mwangalizi wa uchaguzi aliyeidhinishwa na NEC kimaandishi na katika utaratibu uliowekwa.
Uchaguzi huo unafanyika leo baada ya kuahirishwa Juni 16, mwaka huu, baada ya bomu la kutupa kwa mkono kulipuka kwenye mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Agizo la kupiga marufuku kujihusisha na Uchaguzi Mkuu wa Mkoa(Mulongo) na Mkuu wa Wilaya(Mongella) ambao ni makada na wajumbe wa Kamati za Siasa na Halmashauri za Mkoa na Wilaya za CCM, limekuja wakati kukiwa na tuhuma kutoka kwa vyama vya upinzani, hasa Chadema kuwa wanatumia nyadhifa zao kukibeba chama tawala.
Akizungumzia kunusurika kuwekwa rumande, Heche alisema kutokana na majibu ya polisi wao wakiomba wapewe hata fursa ya kuandika maelezo kuhusu tukio hilo au wapewe polisi kwenda kuzikamata gari hizo, lakini waligomewa, ndipo likatolewa agizo la kukamatwa kuwekwa rumande kwa Lema.

WANAJESHI SABA WA TANZANIA WAUWAWA

Dar es Salaam. Wanajeshi saba wa Tanzania, ambao ni miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa, cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wanadaiwa kuwa wameuawa.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kwamba wanajeshi hao wa Tanzania, wamekufa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaopigana na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, miili yao wanajeshi hao bado ipo nchini Sudan ikisubiri taratibu za kusafirishwa kuletwa nchini.
Hii ni mara ya kwanza kuripotiwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kufa kwa wakati mmoja.
Agosti mwaka jana wanajeshi watatu wa Tanzania huko Darfur waliripotiwa kuuawa kwenye tukio kama hilo.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , Kanali Kapambala Mgawe alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu vifo vya wanajeshi wa Tanzania huko Darfur, alisema kuwa naye amesikia, lakini hana taarifa rasmi kwa mujibu wa taratibu za kiofisi.
Hii ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa katika Jimbo la Darfur, ambapo Agosti mwaka jana, Kanali Mgawe alinukuliwa na vyombo vya habari akithibitisha kutokea kwa vifo vya askari watatu ambao gari lao lilizolewa na maji walipokuwa wakivuka mto uliokuwa umefurika maji.
Kanali Mgawe aliwataja askari hao kuwa ni Sajini Julius Chacha, Sajini Anthony Daniel na Koplo Yusuph Said na kwamba askari wengine walinusurika baada ya kuogolea.
Tanzania ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani jimbo la Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa kulinda amani katika jimbo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Tanzania wametawanywa kwenye miji ya Khor Abeche na Muhajeria kusini mwa Darfur.
Aprili mwaka huu Tanzania ilipeleka wanajeshi wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupambana na kikundi cha waasi wa nchi hiyo M23 kinachopigana kuiangusha serikali ya DRC.
Majeshi ya Tanzania yalipelekwa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania inaungana na nchi za Afrika Kusini na Malawi kukamilisha kikosi cha wanajeshi 3,000. Tanzania imepeleka wanajeshi 850.

MOTO WASABABISHA KUFUNGWA UWANJA WA NDEGE KWA MUDA

Ndege ya aina ya Boeing 787 inayomilikiwa na Shirika la ndege la Ethiopia katika uwanja wa Heathrow
Shughuli katika uwanja wa ndege wa Heathrow zimekwama kwa muda baada ya ndege moja ya shirika la ndege la Ethiopia aina ya Boeing 787 Dreamliner kushika moto.
Safari zote za ndege katika uwanja huo zilisitishwa kuanzia saa kumi na nusu.
Kwa mujibu wa msemaji wa mamlaka ya uwanja wa ndege wa Heathrow, hakuna abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo wakati wa tukio hilo.
Mapema mwaka huu ndege hamsini aina ya Dreamliners, zilisimamishwa kufanya kazi kutokana na matatizo ya mtambo wa Battery.
Mwezi April, ndege moja ya shirika la ndege la Ethiopia, ambalo limesemekana kuwa ndilo lililopata matatizo katika uwanja wa Heathrow, ilisafiri kutoka Adis Ababa hadi Nairobi kwa mara ya kwanza tangu mwezi Januari.
Picha zilizochapishwa kwenye mtandao wa Kijamii wa Twitter, zimeonyesha ndege moja katika uwanja huo ikiwa imezingirwa na magari ya kuzima moto.
Wafanyakazi wa idara ya kuzima moto ya baraza la mji wa London wamesema kuwa walikuwa tayari kushirikiana na maafisa wa kitengo cha kupambana na mikasa ya moto katika uwanja huo.

MAREKANI NA UJERUMANI WATAKA MURSI AWE HURU

Matukio ya Afrika

Marekani, Ujerumani zataka Mursi aachiliwe

Kundi la Udugu wa Kiislamu limeitisha maandamano makubwa ya umma nchini Misri siku ya Jumatatu huku Marekani ikiungana na Ujerumani kutaka kuachiliwa huru kwa rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Mursi.
Wito wa Udugu wa Kiislamu umetolewa masaa kadhaa baada ya maelfu ya wafuasi wa Mursi kuingia mitaani kwenye maandamano ya amani ya kudai kuachiliwa kwa kiongozi wao mjini Cairo.
"Jumatatu ijayo, Mungu akipenda, umma mkubwa utakusanyika kwenye viwanja vyote vya Misri dhidi ya mapinduzi haya ya kijeshi. Misri huamua kupitia kura na maandamano maandamano ya amani. Hakuna yeyote, kundi lolote au taasisi ya kijeshi itakayolazimisha maamuzi yake kwa watu wa Misri," amesema Essam El-Erian wa chama cha Uhuru na Haki, ambacho ni tawi la kisiasa la Udugu wa Kiislamu.
Kundi la Udugu wa Kiislamu limekataa aina yoyote ya mazungumzo ya kisiasa tangu wakati huo, likishikilia kwamba ni lazima Mursi arejeshwe madarakani.
Marekani, Ujerumani zataka Mursi aachiliwe
Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013. Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013.
Siku ya Ijumaa, Marekani ilitoa wito kwa jeshi la Misri kumuachia Rais Mohamed Mursi, ikisema inaungana na Ujerumani ambayo ilitangulia kutoa wito kama huo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Jen Psaki, alisema nchi yake inakubaliana na Ujerumani katika hilo na kwamba ilitoa ombi hilo hadharani. Licha ya serikali ya mpito kusema kwamba Mursi yuko salama, lakini hajaonekana hadharani tangu alipopinduliwa na jeshi tarehe 3 Julai.
Psaki alisema Marekani inataka kuondolewa kwa usiri juu ya taarifa za wapi alipo Mursi, ambapo Ujerumani ilipendekeza kwamba taasisi inayoaminika, kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu, ipewe fursa ya kumuona na kumuhudumia Mursi.
Maandamano yapamba moto
Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013. Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013.
Maandamano tafauti ya kumuunga mkono na kumpinga Mursi yalifanyika mjini Cairo siku ya Ijumaa (tarehe 12 Julai), kwa njia ya amani licha ya hofu za awali kwamba yangelikumbwa na machafuko.
Magharibi ilipoingia, maelfu ya wafuasi wa Mursi kwenye mitaa kadhaa ya Cairo waliswali na kukata swaumu zao, ikiwa ni Ijumaa ya kwanza tangu kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo katika uwanja maarufu wa Tahriri na nje ya kasri ya rais ya Ittihadiyya, mamia ya waandamanaji wanaompinga Mursi walifutari pamoja.
Wafuasi wa Mursi wamekuwa wakiandamana pia nje ya msikiti wa Rabaa al-Adawiya katika mji wa Nasr, ambako wakiwa wamebeba Qur'an na bendera za Misri, wanasikikana wakipiga mayowe ya kuyalaani mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia.
"Tutaendelea kupambana," kiongozi wa ngazi za juu wa Udugu wa Kiislamu, Safwat Hegazi aliuambia umma siku ya Ijumaa. "Tutakaa hapa kwa mwezi mmoja au miwili, au hata mwaka mmoja au miwli. Hatutaondoka hadi rais wetu, Mohamed Mursi, arudi."
Hayo yanatokea katika wakati ambapo waziri mkuu wa serikali ya mpito, Hazem el-Beblawi, anatarajiwa kuliapisha baraza jipya la mawaziri wiki ijayo.
Baraza hilo lina jukumu la kuutekeleza mpango wa jeshi kuelekea utawala wa kiraia, baada ya jeshi kumpindua rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia hapo tarehe 3 Julai

KUELEKEA UCHAGUYI MKUU ZIMBABWE

Matukio ya Afrika

Mugabe, Tsvangirai uwanjani

Mahasimu wa kisiasa nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai wamenadi sera zao kwa malengo ya kulikwamua taifa hilo kiuchumi, ikiwa ni jitihada za kuwavutia wapiga kura kabla ya Machi 31.
Kwa mujibu wa tathmi ya shirika la habari la Ufaransa AFP mahasimu hao "walirindima", mwishoni jumamosi ikiwa zimebaki wiki si zaidi ya tatu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa taifa hilo, unaotarajiwa kufikisha kikomo serikali yao ya mizengwe iliyolazimishwa kuundwa kutokana na uchaguzi wenye vurugu wa 2008.
Akizungumza katika kampeni yake katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ya almas kwa upande wa mashariki, Tschangirai alisema " Chaguo ni rahisi sana, ni kati ya serikali iliyoshindwa kwa zaidi ya miaka 33 na ahadi mpya ambazo ziko wazi kabisa" Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 alizungumza katika mji wa Mutare akimtolea mfano rais Mugabe kuwa mwenye kutaka kuhodhi madaraka.
Mugabe na sera za uzawa
Supporters cheer Zimbabwean President Robert Mugabe as he arrives to launch his ruling ZANU PF party's election manifesto in the capital Harare July 5, 2013. Zimbabwe's Constitutional Court rejected a series of government appeals on Thursday to delay a July 31 general election in order to allow more time for reform of the security forces and state media. REUTERS/Philimon Bulawayo (ZIMBABWE - Tags: POLITICS ELECTIONS) Wafuasi wa Robert Mugabe
Mugabe mwenye umri wa miaka 89, akiwa amevalia kanzu nyeupe huku ameshika biblia mkononi alijitokeza mbele ya maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika katika eneo la kanisa moja huko mjini Marange, umbali wa kilometa 200, mashariki mwa mji mkuu Harare. Akinukuliwa na AFP kiongozi huyo mkongwe barani Afrika alisema"Tulifanya makosa 2008 kumchagua mtu ambae anapenda Wazungu. Kumpigia kura mtu ambae anataka kuwarejesha wazungu na ambae anafikiri haiwezekani kuwepo kwa maendeleo nchini Zimbabwe bila kuhusishwa watu hao" Alisema rais Mugabe.
Katika kunadi sera zake kiongozi huyo mkongwe alilenga masuala ya uzawa, au sera za uzawa na kuwawezesha watu weusi akisema kwamba Zimbabwe lazima imiliki sehemu kubwa ya rasilimimali yake. Kwa upande wake Tsvangirai ameahidi kurekebisha uchumi, kufufua viwanda na kuvutia uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa ajira kwa vijana nchini humo.
Almas kwa Wazimbabwe wote
Zimbabwe opposition Movement For Democratic Change (MDC) leader Morgan Tsvangirai speaks at the launch of his party's election campaign in Marondera, about 70 km (43 miles) east of Harare, July 7, 2013. Tsvangirai, launching his third campaign to unseat veteran President Robert Mugabe, said nothing had been achieved to ensure a fairer vote but even God now wanted Mugabe to go. REUTERS/Philimon Bulawayo (ZIMBABWE - Tags: POLITICS ELECTIONS) Mgombea urais Zimbabwe Morgan Tsvangirai
Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi waliovaa fulana nyekundu zenye picha yake. Tsvangirai ameahidi kufanikisha uwazi katika uchimbaji wa madini ya almas. Nikimunukuu kiongozi huyo wa upinzani hapa alisema " Wapi zinapokwenda fedha za almas? Tunafahamu tukipata fedha zote kutoka katika madini hayo tunaweza kuunda ajira mpya laki moja. Alisema katika mkutano wake wa kampeni uliyofanyika katika uwanja wa Mutare, uliyopo kilometa 250 mashariki mwa Zimbabwe.
Aliongeza kusema kama mapato yote kutoka katika madini hayo yangefika moja kwa moja katika mikono ya serikali wangaliweza kulia walimu na wanajeshi na sio kama ilivyo sasa ambapo mapato hayo yanawanufaisha watu wachache. Kama atapewa ridhaa ya Wazimbabwe kuongoza taifa hilo Tsvangirai ameahidi kupitia upya mikataba yote katika sekta ya madini kwa kuwa ya sasa inatoa mianya ya kuendelea kwa vitendo vya rushwa.
Aidha katika kampeni yake rais Robert Mugabe amepinga ndoa za jinsia moja kuwa zinakwenda kinyume na utamaduni wa Afrika na kuikosoa vikali kauli ya rais Obama barani wakati alipozulu Afrika kuhimiza waafrika kuheshimu haki za mashoga. Mugabe alisisitza kauli yake hiyo kwa kusema ndoa ni ya mwanamke na mwanaume ambapo matunda yake ni kuzaliwa watoto.
Katika uchaguzi uliyopita Zimbabwe iligubikwa na visa vya umwagikaji damu. Tsvangirai alijiondoa katika kinyanganyiro hicho pamoja na cha mwaka 2008 pamoja na kuibuka na ushindi katika duru ya kwanza. Uchaguzi wa mwezi huu unatajwa kuwa wenye kuweza kuifikisha serikali ya mseto nchini humo ambayo imesababisha kudidimia kwa uchumi.

MAANDAMANO TENA MISRI

Wafuasi wa rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi
Wafuasi wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi wamefanya maandamano makubwa mjini Cairo, huku waumini wa dini ya Kiislamu wakiadhimsiha Ijumaa ya kwanza tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadan.
Wafuasi wa kiongozi huyo wa vugu vugu la Muslim Brotherhood walijikusanya Mashariki mwa mji huo, kushinikiza utawala wa kijeshi kumrejesha madarakani kiongozi wao.
Wapinzani wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.
Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema vuguvugu la Muslim Brotherhood huenda liliwatenga raia wengi wakati wa utawala wa Morsi, lakini bado raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi kuingilia masuala ya siasa.

Marekani kutuma ndege za kivita Misri

Siku ya Alhamisi serikali ya Marekani, ilitoa wito kwa utawala mpya wa Misri, kusitisha harakati zake za kuwakamata wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood na kuonya dhidi ya kulenga kundi lolote.
Wanajeshi wakishika doria mjini Cairo
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.
Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri.
Marekani inatarajiwa kupeleka ndege nne za kivita aina ya F-16 nchini Misri, lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini.
Serikali ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia mapinduzi.
Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa madarakani.