Masanduku ya kuhesabia kura uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha
Kwa ufupi
Mbali ya NEC kupiga marufuku viongozi hao wa kisiasa
kukaribia vituo hivyo, uchaguzi huo umekumbwa na matukio kadhaa
likiwamo la Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Taifa Chadema(Bavicha), John Heche,
kunusurika kuswekwa rumande jana
Mbali ya NEC kupiga marufuku viongozi hao wa
kisiasa kukaribia vituo hivyo, uchaguzi huo umekumbwa na matukio kadhaa
likiwamo la Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Taifa Chadema(Bavicha), John Heche,
kunusurika kuswekwa rumande jana.
“RC na DC hawana haki wala mamlaka ya kujihusisha
kwenye zoezi na shughuli za upigaji kura. Mwenye dhamana, wajibu na haki
ya shughuli zote za upigaji kura ni Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni
mwakilishi wa NEC pamoja na maofisa wengine wanaotambuliwa kisheria,”
alisema Mwenyekiti wa NEC Jaji Damian Lubuva jana.
Lema na Heche walinusurika kuswekwa rumande baada
ya kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha, wakishinikiza jeshi
hilo, kukamata magari matatu waliyodai kuwa ni ya Chama Cha
Mapinduzi(CCM) na kubadilishwa namba yakihofiwa kwamba huenda yakatumika
kuvuruga uchaguzi wa leo.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea jana asubuhi
baada ya viongozi hao, kufika polisi na kutoa taarifa hiyo, wakieleza
kuwa lakini waliambiwa waondoke kwa kuwa gari kubadili namba siyo kosa
ambapo pia walitakiwa kumtaja aliyewaeleza kama magari hayo yatatumika
kufanya uhalifu.
Aidha, viongozi wa vyama vyote vya siasa ambao sio
mawakala wala wagombea, wamepigwa marufuku kuingia kwenye vituo vya
kupigia kura, wala kujihusisha kwa namna yoyote na zoezi la upigaji kura
badala yake wakiwa ni wakazi wa kata husika kupiga kura na kuondoka
maeneo hayo.
Mwenyekiti wa NEC, alitoa tamko la kuzuia viongozi
hao jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mipango na
mikakati ya tume yake katika kufanikisha zoezi hilo linalofanyika baada
ya kuahirishwa mara mbili.
Mbele ya makamu wake Jaji Mkuu mstaafu wa
Zanzibar, Jaji Hamid Mohamoud Hamid, Jaji Lubuva alitaja orodha ya watu
12 wenye haki kisheria kuingia kwenye vituo vya kupigia kura na
kujihusisha na zoezi la upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura kuwa ni
msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi wa kituo, mawakala wa vyama na
wapiga kura.
Wengine ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, mgombea, mjumbe
wa NEC, Ofisa wa NEC, Mratibu wa NEC mkoa, askari polisi au mtu yeyote
anayehusika na usalama katika kituo cha kupiga kura, mtu anayemsaidia
mpigakura asiyejiweza na mwangalizi wa uchaguzi aliyeidhinishwa na NEC
kimaandishi na katika utaratibu uliowekwa.
Uchaguzi huo unafanyika leo baada ya kuahirishwa
Juni 16, mwaka huu, baada ya bomu la kutupa kwa mkono kulipuka kwenye
mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Agizo la kupiga marufuku kujihusisha na Uchaguzi
Mkuu wa Mkoa(Mulongo) na Mkuu wa Wilaya(Mongella) ambao ni makada na
wajumbe wa Kamati za Siasa na Halmashauri za Mkoa na Wilaya za CCM,
limekuja wakati kukiwa na tuhuma kutoka kwa vyama vya upinzani, hasa
Chadema kuwa wanatumia nyadhifa zao kukibeba chama tawala.
Akizungumzia kunusurika kuwekwa rumande, Heche
alisema kutokana na majibu ya polisi wao wakiomba wapewe hata fursa ya
kuandika maelezo kuhusu tukio hilo au wapewe polisi kwenda kuzikamata
gari hizo, lakini waligomewa, ndipo likatolewa agizo la kukamatwa
kuwekwa rumande kwa Lema.

No comments:
Post a Comment