Powered By Blogger

Translate

Thursday, July 18, 2013

MABOMBA YA GESI YAFIKA MTWARA


Mabomba maalu kwa ajili ya kusafirisha gesi 
Mtwara. Meli kubwa kutoka China tayari imetua katika Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kushusha mizigo ya mabomba ya gesi ili kuanza kwa kazi ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mmoja wa watumishi ndani ya Bandari ya Mtwara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema zaidi ya magari 20 yanatakiwa kupakua mzigo wa mabomba zaidi ya 4,000 kutoka bandarini hapo na kusafirishwa kwenda Kiranjeranje Lindi kwa ajili ya zoezi zima la ujenzi wa bomba hilo.
“Hayo magari mliyoyaona ni miongoni mwa zaidi ya magari 20 yanayokuja kupakua mzigo wa mabomba ambayo ni zaidiya 4,000 kwa ajili ya kuyapeleka maeneo mbalimbali ikiwemo Kiranjeranje Lindi kwa ajili ya kufanikisha zoezi la ujenzi wa njia ya kusafirisha gesi, upakiaji unaendelea hapa Mtwara na Dar meli inapakuwa mzigo ili kupelekwa kwenye maeneo husika na upakuaji kwa mikoa yote unaendelea kwa amani,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa madereva wa magari maalumu kwa ajili ya kupakua mzigo wa mabomba,alisema wametokea Dar es Salaam na hii ni zabuni maalumu waliyoipata kwa ajili ya maandalizi ya kupokea mizigo na kupeleka yanakotakiwa hapo baadaye baadaye baada ya kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
“Hivi sasa tunaenda kupakiza mzigo kwa ajili ya maandalizi tukisubiri siku ambayo wahusika wakuu watakaokabidhiwa,ili na sisi tuanze zabuni yetu ya usafirishaji kuyapeleka yanakohitajika, “ alisema
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo Muhongo alisema tayari meli ilitua katika bandari ya Dar es Salaam na meli kubwa imetua Mtwara kwa ajili ya kushusha mzigo wa mabomba na watakapomaliza yatakabidhiwa na kupokewa kwa heshima kama alivyofanya waziri mkuu jijini Dar es Salaam juzi (Jumapili)
“ Kwa mtu anayejua uchumi kitu kitakachotutolea umaskini ni hii gesi, mimi ninashangaa watu wa Mtwara wahoji kwa nini mizigo mingine ishushwe Dare es Salaam badala ya Bandari yaMtwara, hata kwa barabara wengine wanaanzia Dar na wengine wanaanzia Mtwara halafu wanakutana, hivyo sioni sababu ya kusafirisha kwa magari baada ya kushusha mizigo yote Mtwara ni kwa nini tuharibu barabara ?” alihoji Profesa Muhongo.
Sudi Mohammedi alisema kitendo cha serikali kwenda kushusha mizigo mingine katika Bandari ya Dar es Salaam ni kuonyesha ni kwa kiasi gani viongozi wasivyoithamini Mtwara kwa kuiacha bandari hiiyo.
Kabla ya kupita kwa magari hayo ya kubeba mizigo maeneo ya Bima, vilianza vifaru vikifuatiwa na gari kubwa lililobeba wanajeshi lililokuwa likizunguka katika baadhi ya maeneo mbalimbali mkoani hapa.

MAOFISA WA WIZARA YA FEDHA MAHAKAMANI

Share bookmark Print Email Rating
 
0
Share
Dar es Salaam. Maofisa wawili wa Wizara ya Fedha wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Wanatuhumiwa kwa ufisadi wa fedha za utoaji wa matangazo na habari kwa vyombo mbalimbali vya habari.
Maofisa waliopandishwa kizimbani ni pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Ernest Simon Mwakitalu na Ofisa Ununuzi, Liipu Neligwa ambao walisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Wakati maofisa hao wawili wakipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo, wengine wawili ambao walitakiwa kupandishwa kizimbani, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Ingiahedi Mduma na Mkurugenzi wa Kampuni ya And- Line (2000) International, Daniel Ukwaya hawakuwapo mahakamani hivyo, mashtaka dhidi yao hayakusomwa hadi watakapokamatwa.
Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 19. Shtaka moja ni kula njama kutenda kosa, mashtaka manane ya kutumia nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri.
Mengine ni shtaka moja la matumizi mabaya ya madaraka, mashtaka manane ya kughushi, shtaka moja la ubadhirifu na shtaka moja la kusababisha hasara ya Sh19.8 milioni, ambalo ni shtaka mbadala kwa wote.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Swai alisema washtakiwa hao walitenda makosa hayo kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai, 2009.
Wakili Swai alidai kuwa washtakiwa hao walisaini hati za ununuzi zenye taarifa za uongo kwa lengo la kuonyesha kuwa Kampuni ya And Line (2000) International ilipewa fedha kwa ajili ya vipindi vinane vya matangazo katika vyombo vya habari vya redio, magazeti na runinga.
Alidai kuwa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari zilihusu maonyesho ya 33 ya Biashara ya Kimataifa yaliyofanyika Dar es Salaam katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Kilwa Road, kuanzia Juni 28 hadi Julai 10, 2009, kwa thamani ya Sh19.8 milioni, jambo ambalo si kweli.
Baada ya kuwasomea mashtaka, Wakili Swai alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa ambayo washtakiwe wengine watakuwa wamekamatwa ili wasomewe maelezo ya awali kwa pamoja.
Washtakiwa waliokuwapo mahakamani jana walikana tuhuma dhidi yao na waliachiwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni, kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika, ambao pia walisaini hati ya dhamana ya kiasi hichohicho.
Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba hadi Agosti 15, mwaka huu itakapotajwa tena.

HAPPY BITHDAY MANDELA

Share bookmark Print Email Rating
Raia wa Afrika Kusini akiwa na bango la kumtakia kheri ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Mstaafu wa nchi hiyo, mjini Polokwane nchini humo. 
Johannesburg: “Happy birthday Mzee Madiba.” Rais wa kwanza na mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo anatimiza umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.
Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern Cape na ametumia zaidi ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na usawa wa wananchi wa Afrika Kusini.
Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.
Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’ ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.
Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine ambao ni wahitaji katika jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo ambaye ni alama ya dunia.