Sunday, June 30, 2013
WABUNGE WAINGANGANIA SSERIKALI
Dodoma. Wabunge wa CCM jana waliungana na Kambi Rasmi ya Upinzani kuing’ang’ania Serikali kwa kuupinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013/2014 uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakitaka kufanywa mabadiliko mbalimbali ikiwamo kuondoa ongezeko la kodi katika mafuta ya petroli kwa manufaa ya wananchi.
Kadhalika, Kamati ya Bajeti imeonyesha kutofautiana na Waziri wa Fedha katika mapendekezo mbalimbali ya muswada huo ikitaka pia kupunguzwa kwa kodi ya mafuta, uagizaji magari huku mwenyekiti wa kamati hiyo akisema kuwa msingi wa mapendekezo yao ni kupunguza gharama za maisha na mfumuko wa bei kwa wananchi.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alipima upepo na kuamua kurudisha kwenye Kamati Muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria za Kodi, na sasa sheria hizo zitapitishwa leo bungeni badala ya jana.
Muda mfupi baada ya kuanza kuchangiwa ndani ya Ukumbi wa bunge jana jioni, Makinda alisimama na kuwatangazia wabunge muswaada huo urudishwe tena katika kamati ambako wabunge waliokuwa wametoa mapendekezo ya marekebisho waliungana na Kamati ili kutoa ufafanuzi wa mapendekezo yao.
Aidha wabunge hao pamoja na Spika wa Bunge waliusifu na kuunga mkono muswada mbadala uliowasilishwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, uliosomwa na mbunge wa Viti Maalumu Christine Mughwai Lisu kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe. Mbali na kuitaka Serikali kuondoa ongezeko la kodi ya mafuta, simu, magari na kupunguza misamaha ya kodi walisema kuwa kitendo cha Serikali kutofuata ushauri wa wabunge kuhusu vyanzo vingine vya mapato, kinawazidishia maisha magumu Watanzania.
Mapendekezo hayo ya wabunge, Kamati ya Bajeti na Kambi ya Upinzani yakipita yataweza kumpatia nafuu mwananchi wa kawaida, huku Serikali ikilazimika kujielekeza kwenye vyanzo vingine vya mapato vilivyoainishwa kwenye bajeti, wabunge wakivitaja baadhi kuwa ni pamoja na kodi katika kampuni za madini, kampuni za simu ili kutimiza malengo ya bajeti yake inayofikia Sh18.2 trilioni.
Akichangia muswada huo ambao mjadala wake ulihitimishwa jana jioni, kabla ya leo Bunge kukaa kama kamati na kuupitia kifungu kwa kifungu Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey zambi alisema: “Sikubaliani kabisa na ongezeko lolote la mafuta na dizeli, hayo yanaongeza moja kwa moja ugumu wa maisha kwa Watanzania.”
Aliongeza akihoji: Serikali ya CCM ndiyo ipo madarakani, wananchi waliichagua kwa kura nyingi, sasa kwa nini izibe masikio kwa wananchi iliyowachagua? Iwasikilise basi, tuondoe tozo zote katika mafuta.”
Kuhusu misamaha ya kodi mbunge huyo alisema kuwa inashangaza kuona kwamba wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CIG) alishauri misamaha ipinguzwe lakini Seikali inaongeza.
“Katika misaha ya kodi hapa kuna vimemo vya wakubwa ni vingi, huyu mpe msamaha, Yule mpe msamaha,” alisema Zambi akiwatuhumu baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali kwa kuhusika na mashinikizo ya kusamehe kodi.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema kupandisha tozo katika ndege hakuendani na kasi ya sasa ya Serikali kujenga viwanja vya ndege maeneo mbalimbali nchini.
“Hii itasababisha taifa kuwa na ndege mbovu jambo ambalo litasababisha ajali za ndege na kuwaumiza Watanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment