Powered By Blogger

Translate

Tuesday, July 2, 2013

OBAMA NA UCHUMI WA AFRIKA

Rais wa Senegal, Macky Sall akimkaribisha Rais wa Marekani, Barack Obama katika Ikulu ya Dakar, Alhamisi iliyopita. Kushoto ni mke wa Obama, Michelle. 
Share

Sera ya Mpango wa Rais wa Kupambana na Malaria na HIV/AIDS (PEPFAR) ulibuniwa wakati wa Rais  George W Bush na umeendelea kwa misingi hiyo wakati wa Rais Obama na ziara yake hii italenga zaidi eneo hilo.
Ujio wa Rais Barack Obama barani Afrika kwa mara ya pili, na safari hii akikaa barani humu kwa takriban wiki moja, ni hatua inayongojewa kwa shauku kubwa, lakini ambayo wafuatiliaji wa habari na wataalamu wa uhusiano kati ya Afrika na Marekani wanashindwa kusema nini hasa cha kutegemea.
Tofauti na ziara ya Rais Xi Jinping wa China hivi karibuni, tena aliyofanya akianza kuingia madarakani - ya kwanza duniani kuacha safari tangulizi ya Russia, ‘mtalaka’ wa China katika sera za Kikomunisti za karne iliyopiga, ziara ya Obama haina matazamio ya miradi mikubwa ya ujenzi, uwekezaji au vinginevyo. Ni wazi Afrika ni muhimu zaidi kwa China hivi sasa kuliko ilivyo kwa Marekani na itabaki hivyo.
Wanaofuatilia takwimu za biashara wanasema kuwa China imeshaipiku Marekani na nchi za Ulaya kama mshirika mkuu wa biashara na Afrika, ila Ulaya ikiungwa pamoja kama Umoja wa Ulaya (EU) bado ina biashara kubwa zaidi na Afrika kuliko China.
Marekani kwa maana hiyo ni ya tatu, lakini ni ya pili kwa nchi moja moja, ingawa umuhimu wake kwa nchi za Afrika una mapana zaidi ya jinsi hizo takwimu zinavyoonyesha.
Nchi hiyo ina hisa takriban asilimia 25 ya vyombo vya fedha vya kimataifa, hasa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, kwa hiyo uhusiano wake na Afrika kwa sehemu kubwa unakwenda kimya kimya, kama sehemu ya kazi za taasisi za kimataifa, si moja kwa moja kama uhusiano bayana.
Ukilinganisha na China, tofauti kubwa kati ya Marekani na China kwa Afrika na ndiyo tofauti inayoonekana katika ziara za viongozi wakuu wa nchi hizo barani Afrika, ni kuwa uhusiano na China ni wa kimkataba na biashara ya ana kwa ana. Uhusiano na Marekani  una mizizi katika mifumo ya biashara iliyopo duniani na sera zake zinajulikana, hivyo unaweza kusoma mapitio na majadiliano kadhaa kuhusu ujio wa Rais Obama barani Afrika usione chochote kuhusu uhusiano huo. Sababu ni kuwa hayaamuliwi katika ziara kama hizi, ila ni sehemu ya usawiri-mifumo ya biashara kimataifa, mielekeo ya kisera inayofuatiliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na mifumo ya kudumu inayokubaliwa na Bunge la Marekani.
Wakati kinachotajwa ni mikopo ya China kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, ni rahisi kusahau kuwa mwelekeo wa kukuza uchumi kwa mauzo ya nje kumeinuliwa sana na sheria ya Marekani ya AGOA (African Growth and Opportunity Act) ambayo kwa miaka 10 sasa imekuwa ufunguo wa nchi kuingia katika soko hilo. Tofauti kati ya nchi imetokana na viwango vya ufanisi ndani ya nchi husika, na hapo ndipo zinapoonekana tofauti kati ya wale wanaotazamia mengi sana kwa ujio wa Rais Obama, na wale wanaotumia mifumo iliyopo ya biashara na Marekani.
Kwa mfano, Kenya inauza mara kumi au zaidi katika soko hilo ukilinganisha na Tanzania, ila ziara ya Obama ni kwa Tanzania na siyo Kenya; yupi mshirika halisi?
Mwelekeo wa Marekani katika biashara na Afrika unatofautiana na China kimsingi kwa sababu Marekani imejikita katika kuboresha uwezo wa Afrika kufanya biashara na kuvuta mitaji, ambayo itaboresha uwezo wa uzalishaji, ufanisi katika sekta tofauti, na upana zaidi wa sayansi na teknolojia. Marekani haitofautiani na Ulaya katika suala hilo ingawa Ulaya imechukua muda kuoanisha ushirikiano na Afrika katika mifumo ya kimataifa ya biashara kwa jumla, wakati Marekani ndiye mlinzi halisi wa mifumo hiyo.
Hivyo Umoja wa Ulaya unachukua muongo mmoja kujadiliana na Afrika nini cha kufanya baada ya uhusiano maalumu ya mkataba wa Lome kuanzia mwaka 1973 yalipoisha kwa shinikizo la Marekani mwaka 2007.
Marekani kwa upande wake haina muda wa kufanya milolongo ya mijadala na nchi za Afrika kupambanua sera zake, bali inaunda sera ndani ya michakato ya sera za vyama vya Republican na Democratic, na kwa jumla ikishaundwa sera inakuwa ya kitaifa, haibadiliki Serikali ya chama kingine ikiingia madarakani.

No comments: